My360 Helper


Kumbukumbu Za Ukoo Wa Yesu Kristo

(Luka 3:23-38)

1Habari za ukoo wa Yesu Kristo mwana wa Daudi, mwana wa Abrahamu:

2Abrahamu akamzaa Isaki,

Isaki akamzaa Yakobo,

Yakobo akawazaa Yuda na ndugu zake,

3Yuda akawazaa Peresi na Zera, ambao mama yao alikuwa Tamari,

Peresi akamzaa Hesroni,

Hesroni akamzaa Aramu,

4Aramu akamzaa Aminadabu,

Aminadabu akamzaa Nashoni,

Nashoni akamzaa Salmoni,

5Salmoni akamzaa Boazi, na mama yake Boazi alikuwa Rahabu,

Boazi akamzaa Obedi, ambaye mama yake alikuwa Ruthu,

Obedi akamzaa Yese,

6Yese akamzaa Daudi ambaye alikuwa mfalme.

Daudi akamzaa Solomoni, ambaye mama yake ni yule aliyekuwa mke wa Uria.

7Solomoni akamzaa Rehoboamu,

Rehoboamu akamzaa Abiya,

Abiya akamzaa Asa,

8Asa akamzaa Yehoshafati,

Yehoshafati akamzaa Yoramu,

Yoramu akamzaa Uzia,

9Uzia akamzaa Yothamu,

Yothamu akamzaa Ahazi,

Ahazi akamzaa Hezekia,

10Hezekia akamzaa Manase,

Manase akamzaa Amoni,

Amoni akamzaa Yosia,

11wakati wa uhamisho wa Babeli, Yosia alimzaa Yekonia na ndugu zake.

12Baada ya uhamisho wa Babeli:

Yekonia alimzaa Shealtieli,

Shealtieli akamzaa Zerubabeli,

13Zerubabeli akamzaa Abiudi,

Abiudi akamzaa Eliakimu,

Eliakimu akamzaa Azori,

14Azori akamzaa Sadoki,

Sadoki akamzaa Akimu,

Akimu akamzaa Eliudi,

15Eliudi akamzaa Eleazari,

Eleazari akamzaa Matani,

Matani akamzaa Yakobo,

16naye Yakobo akamzaa Yosefu ambaye alikuwa mumewe Maria, mama yake Yesu, aitwaye Kristo.

17Hivyo, kulikuwepo na jumla ya vizazi kumi na vinne tangu Abrahamu mpaka Daudi, vizazi kumi na vinne tangu Daudi hadi wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli, na vizazi kumi na vinne tangu wakati wa uhamisho kwenda utumwani Babeli hadi Kristo.

Kuzaliwa Kwa Yesu Kristo

(Luka 2:1-7)

18Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana kuwa na mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 19Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.

20Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema, “Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. 21Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka dhambi zao.”

22Haya yote yalitukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema: 23“Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli”: maana yake, “Mungu pamoja nasi.”

24Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake. 25Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ Hakimiliki © 1984, 1989, 2009, 2015 na Biblica, Inc. Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version™ Copyright © 1984, 1989, 2009, 2015 by Biblica, Inc. “Biblica” ni alama ya biashara iliyosajiliwa katika Ofisi ya Hataza na Alama za Biashara Marekani (United States Patent and Trademark Office) na shirika la Biblica, Inc. Imetumiwa na ruhusa. “Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc. Used with permission.

sajili ya -barua pepe

Sign up for the TWR360 Newsletter

Access updates, news, Biblical teaching and inspirational messages from powerful Christian voices.

Ahsante kwa kujisajili ili kupata ujumbe kutoka TWR360Thank you for signing up to receive updates from TWR360.

Habari inayohitajika haipo

This site is protected by reCAPTCHA, and the Google Privacy Policy & Terms of Use apply.